Taifa masikini ni la watu masikini. Ama, ubora wa kanzu ni nyuzi zake! Katika kitabu chake maarufu cha ‘The Wealth of Nations’, Mwanafalsafa maarufu Adam Smith anasema; “Wakati wote kila mtu binafsi anatumia mtaji alionao kutafuta ajira yenye kipato zaidi. Hakika, ni faida anayoipata yeye binafsi ndiyo anayoitazama, na siyo ile ya jamii. Lakini, anavyoichunguza faida hiyo binafsi, kwa kawaida tu, au kwa kulazimika, inampelekea yeye kupendelea zaidi ajira ambayo huwa ya faida zaidi kwa jamii (Uk. 454).

Katika kitabu hicho Smith anasisitiza kuwa; “…siyo kwa fadhila ya mwenye bucha, muuza mvinyo au muoka mikate ndipo tunategemea mlo wa jioni, bali ni kwa wao kuwa na ndoto na malengo binafsi. Tunajiita ‘sisi’, siyo kwa ule ubinadamu wao, bali ni kwa wao kujipenda wenyewe (Uk.26).

Ametanabaisha kuwa maendeleo ya taifa yanatokana na mtu mmoja mmoja kujipenda na kujipa maisha mazuri. Hivyo, mwalimu akifundisha kwa bidii ili apate ujira zaidi, moja kwa moja wanafunzi wake watafaidika. Fundi rangi naye akifanya bidii, akawa na wateja wengi, taifa litakuwa na nyumba nzuri na biashara ya rangi itakua, na kodi zaidi italipwa. Kipato cha fundi rangi pia kitakua na atajinunulia mahitaji binafsi zaidi, n.k.

Kabla sijandelea zaidi, naomba niulize: “Hivi watanzania ni masikini?….’ Mimi nasema, “kwa kuwa wanashindwa kujipatia mahitaji yao muhimu, na yale ya ziada katika kiasi, ubora na kwa muda muafaka wanapohitaji’… basi wao ni masikini wa kipato….

Kwa zaidi ya miaka 50 sasa tumeshuhudia miradi mingi sana ya kuondoa umasikini nchini. Lakini masikini bado wapo juzi, jana na leo. Tena umasikini umeongezeka. Hakika ni lazima tutambue kuwa uwezo wakuuondoa umasikini upo ndani ya masikini mwenyewe akishirikiana na mifumo tuliyojiwekea. Kamwe uwezo haupaswi kukaa nje yake. Na ili kuuondoa umasikini, ni lazima kila mmoja aweze kujishughulisha na mifumo iliyopo yeye mwenyewe. Hivyo, uwezo ujengwe ndani ya fikra na utashi wa masikini mwenyewe.

Na bila kuuondoa umasikini wa mtu mmoja mmoja, taifa haliwezi kujikomboa. Kukuza kipato cha walio wengi ni lazima kwani kuwa na matajiri wachache kunaleta matabaka na kufifisha uchumi. Mfano, haiwezekani kuwa na tajiri kama Cocacola bila kuwa na watu wenye uwezo wa kununua soda zake. Au kuwa na tajiri mwenye mabasi tele ya abiria, lakini walio wengi wakashindwa kuwa abiria wake…

Ni dhahiri kuwa taifa lililosheheni fukara, lazima liende harijojo. Watang’oa reli, watachukua mafuta ya transfoma, watauana kwa itikadi za uchawi, n.k. ‘Watachakachua’ kila kitu ili waishi. Watakumbwa na magonjwa, vifo, njaa, ujinga, na msongo wa mawazo kusikokwisha. Wakati wote farasi wa maendeleo atakuwa nyuma ya mkokoteni na taifa halitaendelea. Jela patafurika. (Hili nitalizungumza kwa kina siku nyingine).

Tanzania kama zilivyo nchi nyingi masikini duniani, uchumi wake unategemea sana kilimo. Na asilimia 70 ya wakulima wake wanatumia zana duni kuzalisha kidogo katika mashamba madogo. Hii inamaanisha kuwa asilimia 70 ya nguvukazi ‘iko bize’ na kilimo cha Pwagu na Pwaguzi. Kwa msemo wa Juma Nature ‘wanapata njegere mbili kwenye maganda kumi’. Matokeo yake hawana uwezo wa kulipa kodi. Hii ni kusema kuwa, sehemu kubwa ya nguvukazi yetu ‘inachumia tumbo’ na ni mzigo kwa taifa. Ni kama vile asilimia zaidi ya 60 ya mwili wa taifa letu imepooza!!

Ukweli ni kuwa hatuwezi kuruhusu nguvukazi kubwa ya taifa iendelee kujishughulisha na kilimo kisicho na tija, kisichokua, na ambacho familia inalima ekari zile zile, kwa mtindo ule ule miaka nenda miaka rudi toka wazazi wanaoana mpaka leo watoto wanne wanafika sekondari. Shamba ni lile lile, na magunia wanayovuna ni yale yale kwa ekari. Yaani kipato hakiongezeki lakini mahitaji ya familia ya chakula, elimu na afya yanaongezeka. Hii ni inadhihirisha kuwa kuweka malengo ya Milenia ya kupunguza umasikini bila kuongea uwezo wa mtu mmoja mmoja kuzalisha ni ‘uwendawazimu!’

Kwa mtazamo wangu, umasikini wa kipato ni kukosa uwezo wa kununua (kushindwa kununua). Kununua ni muhimu sana katika dunia ya leo kwani hakuna mwanadamu anaeweza kuzalisha mahitaji yake yote mwenye. Tunaishi kwa kuuza na kununua. Hii inafanya dawa ya umasikini wa kipato iwe kupata uwezo wa ‘Kuuza sana’ ili kununua sana. Kwani mtu hawezi kununua sana asipouza sana, labda awe ‘mwizi’ au ‘ombaomba’. Hivyo tunachohitaji kama taifa ni kumjengea kila mtanzania uwezo wa kuzalisha na kuuza maradufu ili tuweze kununua zaidi. Sisi ni masikini kwasababu aidha hatuna tunachouza, au tunauza kidogo sana!..

Swali ni je, watu wetu wanauza nini? Na wanachokiuza kinawapa fedha zaidi au pungufu ya mahitaji yao? Je kina ubora wa kushindana sokoni? Vitu watanzania wanavyoweza kuuza, ni: ujuzi (ajira, huduma), vipaji (sanaa, michezo), nguvu za mwili (vibarua, ulinzi, upagazi), au bidhaa halisi (k.m samani, mazao ya kilimo). Ili wauze kimojawapo katika hivyo, wanahitaji uwezo wa kuzalisha kwa wingi, kwa ubora, kwa wakati, na kwa gharama nafuu! Na ili tufanikiwe, ni lazima tujenge mifumo sahihi, na kulipia gharama zote za kijaamii (social cost).

Kimsingi, tunahitaji kupanua uwezo wa watanzania kutokea ndani mwao. Tujenge mitazamo, fikra na ujuzi sahihi kabla ya kugawa nyenzo na mitaji. Ukweli ni kuwa, kama uwezo wa mtu ni sawa na ujazo wa chupa ya nusu lita, hata tukimzamisha baharini mwaka mzima, kamwe hataweza kukinga maji zaidi ya nusu lita. Na ili akinge maji mengi zaidi, ni lazima ujazo wake uongezeke. Watanzania tunahitaji ujazo mpya. Tuache kukimbilia bahari. Je ujazo wa ndani ni upi? Unajengwaje? (Itaendelea).

Ustawi ni tabia, ni utu

5 thoughts on “Ustawi ni tabia, ni utu

  1. Ubarikiwe dada Vera. Ni uamuzi wa busara wa kuungwa mkono kwa kuamua kuchangia mawazo yako chanya yenye nia dhabiti ya kumsaidia mtanzania na Tanzania.Nakereka sana ni “mipango ya kiuchumi” ya kwenye makaratasi. Tumekuwa mabingwa wa kuandika mipango mkakati miiingi yenye kuzinduliwa kwa mbwembwe lakini zaidi ya nusu ya fungu litaishia kwa wanene wa Masaki na Oysterbay kwenye warsha na semina. May be tuna-copy walichofanya Indonesia au Malaysia au Vietnam bila ku-copy usafi na nia thabiti ya watendaji wake waliofanikisha huko walikofanikiwa.

    Liked by 1 person

    • Asante sana Dr. Mbata. Katika kitabu chao cha “Why Nations Fail: The Origins of Power, Proerity and Poverty”Daron Acemoglu na James Robinson” wameandika kuwa nchi nyingi za Africa zinaendeleza kutekeleza msururu wa miradi isiyo na tija (I.e.”irrelevant development programs”), ambayo inasigina uwezo wa ndani wa kujikwamua toka kwenye umasiki… Shida ni kuwa Kutoka kwenye mazoea hayo kunahitaji ujasiri na uthubutu mkubwa. Ifike mahali miradi na mipango mingine ipimwe kwa undani na wananchi.

      Like

  2. Dada Vera
    Asante kwa mchango wako. Nakubaliana nawe kuwa ili mzalishaji au mtoaji huduma aendelee kufanya hivyo lazima apate faida. Ina maana yapasa kuwe wanunuzi watakaoweza kulipa bei inayomrudishia gharama za uzalishaji na ziada yake ambayo ni faida. Kwa hiyo kuwa na wateja wenye kipato cha kutosha na wanahitaji bidhaa au huduma ni kanuni ya msingi kabisa katika kumwondoa mwananchi kwenye mzunguko wa umaskini. Kwa hiyo hata kama mzalishaji au mtoa huduma angelima kisasa (pamoja na kupewa pembejeo bure na mbegu za kisasa) kama hakuna soko la kumtoa huyu mkulima ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu. Ningekuomba katika mada yako ujaribu kuunganisha hoja hii na ule uzoefu wako wa kuhamasisha ufugaji wa kuku wa mayai Mkoa wa Njombe. Naona kama umepata masomo mazuri ambayo nchi inaweza kujifunza jinsi ya kumkwamua maskini. Wasalaam. nduguyo Lunogelo

    Liked by 1 person

    • Asante sana Dr. Lunogelo. Ni ukweli kuwa umasikini hauwezi kuisha bila kujenga uwezo wa “kununuliana”. Kila mtu awe na kitu cha kuuza (I.e. ujuzi, kipaji, bidhaa, etc), na kisha kuwe na wanunuzi au walaji wenye uwezo wa kununua. Kujenga uchu wa kuagiza na kutumia bidhaa kutoka nje bila kujua uwezo wa ndani wa kununua unajengwaje ni kuongeza umasikini. Mfano, Waalimu wenye mishahara midogo watakuwaje wateja wa Fundi cherehani kijijini? Fundi huyu biashara yake itakuzwa na nini? Nitazingatia ushauri wa kuelezea uzoefu nilioupata Njombe.

      Like

Leave a comment